
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz
Tovuti : www.foreign.go.tz
Nukushi: 255-22-2116600
20 KIVUKONI FRONT,
P.O. BOX 9000,
11466 DAR ES SALAAM,
Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu Viongozi kutoka nje ya nchi watakaohudhuria Sherehe za Kuapishwa kwa Rais wa Awamu ya Tano
Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli ataapishwa rasmi kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 05 Novemba, 2015.
Sherehe hizo ambazo zitafanyika katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam zitahudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda na Wawakilishi mbalimbali kutoka nje ya nchi.
Miongoni mwa Marais watakaohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Mhe. Robert Mugabe, Rais wa Zimbabwe, Mhe.Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Uganda, Mhe. Paul Kagame, Rais wa Rwanda, Mhe. Jacob Zuma, Rais wa Afrika Kusini.
Wengine ni Mhe. Joseph Kabila, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mhe.Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya, Mhe. Filipe Nyusi, Rais wa Msumbiji na Mhe. Edgar Lungu, Rais wa Zambia.
Malawi itawakilishwa na Makamu wa Rais, Mhe. Saulos Chilima huku Namibia ikiwakilishwa na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah. Aidha, Serikali ya China itawakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Tawala.
Vilevile nchi nyingine ambazo zimethibitisha kushiriki na zitawakilishwa na kati ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika au Balozi ni pamoja na Burundi, Comoro, Angola, Botswana, Lesotho, Madagascar na Mauritius.
Nyingine ni Norway, Oman, Sudan Kusini, Sweden, Umoja wa Falme za Kiarabu, Marekani, Uingereza, Shelisheli, Swaziland, Algeria, Misri, Benin, Denmark, Ethiopia, Finland, Ufaransa, Ghana, India, Japan, Kuwait, Uholanzi na Nigeria.
Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na Kikanda waliothibitisha kushiriki au kutuma wawakilishi wao ni pamoja na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC); Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU), Jumuiya ya Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam