Mtu mmoja amekufa kwa kupigwa risasi na wengine wawili kujeruhiwa vibaya baada ya watu wanaodaiwa kuwa ni vikundi vya uhalifu vilivyokuwa na silaha mbalimbali kuvamia mabweni mawili yaliyokuwa na wanafunzi wa chuo kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kulowa na kumwaga mafuta ya petroli na kisha kuyateketeza kwa moto.
Aliyekufa katika tukio hilo limetokea majira ya saa sita usiku katika chuo hicho kilichopo kata ya Magamba wilayani Lushoto ni mlinzi Joseph Shemzigwa(34) ambaye alipigwa risasi ya kichwani na mwingine ni Abuu Rajab(33) pamoja na mtu aliyevamiwa na baadhi ya walinzi wa chuo hicho ambaye hajajulikana mara moja huku akiwa na silaha baridi kama ni miongoni mwa wahalifu hao ambao wote wamelazwa katika hospitali teule ya wilaya ya Lushoto.
Akielezea jinsi walivyovamiwa katika mabweni yao mmoja kati ya wananchuo Benadetha Leon amesema mara baada ya kuvamiwa watuhumiwa wanadaiwa kuwa walianza kuulizana maswali kuwa watumie mbinu gani za kufanya mauaji hayo
kwa kuwachinja kisha kuwateketeza kwa moto ndipo ghafla mmojawapo alipomwaga mafuta ya Petrol ndani ya mabweni yao na kuwasha moto hatua iliyowalazimu kutumia ujasiri wa kupenya katika dirisha dogo la chooni na kukimbia msituni na kufanikiwa kuokoa maisha.Kufuatia hatua hiyo kamati ya ulinzi na usalama mkoa chini ya mwenyekiti wake mkuu wa mkoa wa Tanga ipo wilayani Lushoto kwa ajili ya kushughulikia tukio hilo.