Rais John Pombe Magufuli amesema azma ya serikali yake kuhamia Dodoma haraka iwezekanavyo ipo pale pale huku akiwaonya wale wataong’ang’ania kubaki Dar es Salaaam kuwa watakuwa wamejifukuzisha kazi wenyewe.
Alitoa msimamo huo mjini hapa kwenye mkutano wake wa kwanza wa hadhara mkoani Singida tangu achaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka jana.
Alisema kuwa licha ya kuhamia Dodoma atahakikisha anauza majengo ya Wizara mbalimbali yaliyopo Dar es Salaam kwa mnada ili wale wasiotaka kuhama, wahame kwa lazima.
“Mimi nitahakikisha baada ya kuhamia Dodoma napiga mnada majengo yote ya Wizara na atakayeng’ang’ania kubaki huko ajue hana kazi wala mshahara, hatuwezi kuendelea kukaa miaka hamsini tunaimba tu kuhamia Dodoma wakati hatutekelezi maamuzi yetu hadi wengine wameshatangulia mbele za haki,” alisema.
Na Nathaniel Limu, Manyoni