Ibrahim Ajib akiwa na wachezaji wenzake wakishangilia bao la pili wakati wa mchezo wao dhidi ya Azam FC
Dar es Salaam derby kati ya Azam FC ambao walikuwa wenyeji wa mchezo wa leo dhidi ya ‘mnyama mnyamani’ Simba imemalizika kwa sare ya kufungana magoli 2-2 mchezo uliosukumwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
John Bocco ‘Adebayor’ alianza kuipatia Azam bao la kwanza dakika ya kwanza baada ya mabeki wa Simba kufanya uzembe wa kuokoa mpira uliokuwa unazagaa langoni ambao ulimkuta Farid Musa kisha akatoa pasi kwa nahodha huyo wa Azam ambaye aliukwamisha mpira kambani na kuiandikia timu yake goli la kuongoza mapema kipindi cha kwanza.![]()

Beki wa Simba Hassan Isihaka (kulia) akijaribu kumdhibiti striker wa Azam FC John Bocco
Azam baada ya kupata goli hilo walionekana wameridhika na kuwaacha wekundu wa Msimbazi kutawala asilimia kubwa ya mchezo wakati wa kipindi cha kwanza.
Ibrahim Ajib hakuwaacha mashabiki wa timu yake wasononeke muda wote kwani aliwapa faraja baada ya kuisawazishia timu yake kwa kufunga goli dakika ya 24 kipindi cha kwanza na kuufanya mchezo huo kwenda mapumziko huku timu zote zikiwa sare kwa goli 1-1.![]()

Beki wa Simba Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ akimtoka beki wa Azam FC Shomari Kapombe
Kipindi cha pili Simba waliendeleza mashambulizi langoni mwa Azam lakini walishindwa kufunga magoli kadhaa kutokana na kutokuwa makini kumalizia nafasi zilizokuwa zimetengenezwa.
Dakika ya 69 Ibrahim Ajib alirudi tena kambani kuifungia Simba bao la pili na bao lililoifanya Simba iwe mbele kwa bao 2-1 dhidi ya ‘waoka mikate’ wa Chamazi.![]()

Beki wa Azam FC Shomari Kapombe akijaribu kupiga krosi mbele ya Tshabalala
Wakati kila shabiki wa Simba akiamini timu yao itaibuka na ushindi wa bao 2-1, John Bocco ‘Adebayor’ alizima furaha na shangwe za wana-Msimbazi baada ya kupachika mpira wavuni na kuinusuru timu yake kupoteza pointi zote tatu mbele ya Simba.
Dakika 90 za mchezo huo zikamalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 2-2.